This post is also available in English (here) and Amharic (here).
Mabadiliko ya tabia ya nchi, uharibifu wa mazingira na ueneaji wa mimea vamizi kama Mathenge (Kitaalamu Prosopis juliflora) ni tishio kubwa kwa upatikanaji endelevu wa kipato kwa jamii zinazoishi maeneo makame. Changamoto hizi pia zinaathiri mifumo ya kiikolojia katika kutoa huduma kama malisho kwa mifugo ambayo ni rasilimali muhimu kwa wafugaji na wakulima. Utafiti wa hivi karibuni uliyofanywa na Eschen na wenzake, umeonyesha kuwa ukataji wa mti vamizi aina ya Mathenge na kuirejesha ardhi katika uoto wa asili kutapelekea manufaa makubwa ya kiuchumi kwa jamii, pamoja na kutoa mchango mkubwa katika kupunguza athari kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi katika Kaunti ya Baringo, Kenya.
Mnamo mwaka 2018 jopo la wataalumu lililohusisha wanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) na wanasayansi waliobobea katika nyanja mbalimbali kutoka nchi nne tofauti walihudhuria mafunzo kwenye taasisi ya SESYNC Summer Institute ya Marekani. Mafunzo hayo yalilenga kujifunza mbinu mpya za kisayansi za kuchambua na kuandika maswala ya kijamii na mazingira. Mafunzo hayo yaliiwezesha jopo hilo kushirikiana na kutoa andiko la kisayansi linaloonesha njia mbadala za kudhibiti Mathenge na urejeshaji wa nyasi asilia ili kuboresha afya ya udongo na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa jamii.
Utafiti ulitumia takwimu za kijamii, kiuchumi na kiikolojia zilizokusanywa na wananfunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) kutoka mradi wa Woody Weeds, zikionesha makadirio ya bajeti ya koundoa Mathenge, na faida za kifedha zitokanazo na kuchoma mkaa kutoka kwenye miti iliyoondolewa, upimaji wa udongo ili kutathimini mabadiliko ya ukaa (SOC) baada ya kuondoa Mathenge na kurejesha uoto wa asili wa nyasi. Takwimu hizi zilichambuliwa na kuunganishwa na takwimu nyingine kutoka kwenye mfumo wa satelaiti ambazo zinaonesha ramani ya maeneo yaliyovamiwa na Mathenge.

Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa fedha ambazo jamii imeridhia kugharamia kuondoa Mathenge kwa mwaka, zinatosha kudhibiti mmea huo katika Kaunti ya Baringo. Urejeshwaji wa uoto wa asili katika maeneo yaliyovamiwa na Mathenge utaleta faida kubwa za kiuchumi. Faida za muda mfupi zitatokana na uzalishaji wa mkaa kutoka kwenye miti iliyoondolewa na faida za muda mrefu zitatokana na upatikanaji wa malisho kutoka kwenye nyasi za asili zitakazorejeshwa.
Nyasi hazihitaji mvua nyingi kukua na kukomaa kama ilivyo kwa mazao ya chakula kama mahindi na maharagwe. Katika baadhi ya vijiji kwenye Kauti ya Baringo, upandaji wa nyasi bora kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu umeshaenea, pia wakulima wameanza kuuza nyasi kavu. Kwa kuongezea, urejeshaji wa uoto wa nyasi utasaidia kuboresha uchumi na hali za maisha kwa wanajamii katika maeneo haya kwa kupitia ufugaji.
Ujumuishaji wa takwimu za usambaaji wa mimea vamizi (IAS), gharama za udhibiti, faida za kiuchumi, na historia ya matumizi ya ardhi inaweza kuwa njia sahihi ya kutengeneza mkakati sahihi na halisi katika kuthibiti mimea vamizi. Mikakati hiyo itazingatia gharama zitakazotumika na faiada zitakazopatikana na hivyo kuwasaidia wadau kuchagua njia ambazo ni sahihi, nafuu, rafiki, na zinazowezekana kulingana na mahitaji yao.
Tunahitimisha kuwa, mikakati ya kudhibiti mimea vamizi katika maeneo yaliyo vamiwa iambatane na uboreshaji wa hali ya kiuchumi ya jamii katika eneo husika. Pia, mikakati hiyo itumike kwa mapana zaidi ili kusaidia katika maamuzi ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira, haswa pale penye uhaba wa rasilimali ardhi na fedha, na penye utofauti wa faida na hasara za udhibiti wa hiyo mimea vamizi miongoni mwa wadau.
Read the full Open Access article Prosopis juliflora management and grassland restoration in Baringo County, Kenya: Opportunities for soil carbon sequestration and local livelihoods in Journal of Applied Ecology.
2 thoughts on “Mikakati madhubuti ya kudhibiti Mathenge (Prosopis juliflora) yaonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya wananchi wa Kaunti ya Baringo, Kenya”